Darassa ni hadithi ya mafanikio ambayo kila mdau wa muziki
ataikumbuka kwa mwaka 2016. Na hadithi yake ina funzo kubwa katika namna
ambayo hit song hupatikana. Pengine nilichojifunza zaidi ni kuwa hakuna
formula ya jinsi ya kupata hit.

Kwamba ‘don’t bother, just hit the studio do what you love’ mengine
yatajulikana mbele ya safari, right? Kwasababu wakati mwingine ule wimbo
ambao msanii aliurekodi kwa kujiachia tu studio kuwapa mashabiki wake
zawadi, hugeuka kuwa mkubwa hadi humshangaza yeye mwenyewe. Na wakati
mwingine, wimbo ambao msanii huuwekea mikakati mikubwa, kufanya
uwezekaji wa kufa mtu na promo nzito, hugeuka kuwa ‘flop’ na
‘disappointment’ kubwa.
Kilichotokea mwaka huu kwa Darassa ni mawimbi ambayo kila kona
imeyahisi. Muziki umegeuka kuwa wimbo wa hadhi ya ‘national anthem’ kwa
muda mfupi. Ndio wimbo wenye rotation kubwa zaidi nchini kwa sasa.
Huwezi kuukwepa. Usipousikiliza kwenye redio, utaona video yake kwenye
TV. Usipousikia kwenye baa ya jirani, utausikia kwenye bajaj au bodaboda
inayokatiza wakati ukitembea barabarani. Kwa ufupi katika mzunguko wako
saa 12 za siku, uhakika wa sikio lako kuguswa na mawimbi ya mdundo wake
ni mkubwa, utake ustake au labda uweke pamba sikioni.
Na kwa muda mfupi, Darassa amegeuka kuwa msanii wa rap mwenye show
nyingi. Darassa amegeuka ‘hot cake.’ Hivyo inamlazimu kusafiri muda
mwingi kwaajili ya kutumbuiza. Mfano siku kadhaa zilizopita alikuwa na
show tatu katika mikoa miwili tofauti, Iringa na Shinyanga. Ni katika
safari yake ya kutoka Kahama kwenda Kakola mkoani Shinyanga ndipo yeye
na timu yake walipopata ajali ambayo kama si rehema za Mungu, angegeuka
kuwa #hashtag.
Katika wakati huu ambao Darassa anafanya vizuri, amekuwa akipata
ushauri mwingi kutoka kwa watu wanaotaka afike mbalimbali zaidi na
kwamba asije siku moja akapotea tena baada ya kufika kwenye kilele cha
mafanikio kimuziki. Hofu hiyo haikwepeki sababu kuna mifano mingi ya
watu waliowahi kutoa nyimbo za ukubwa huo lakini leo hii wanapumulia
mashine.
Miongoni mwa ushauri anaoupata ni kuwa apunguze show anazofanya kwa
kuweka dau kubwa zaidi ili kuzichuja. Moja ya waliompa ushauri wa aina
hiyo ni Sebastian Ndege, ambaye katika sehemu ya alichomshauri anasema,
“Usichukue show za mapromoter uchwara waka dissapoint mashabiki wako
kuwatia hasira na kukushusha hadhi. Bora ufanye shows chache lakini za
ukweli, with detailed showcase.”
Mwingine ni Le Mutuz ambaye anamshauri kuwa ni muda wa yeye kuanza
kuchukua malipo ya shilingi milioni 15 hadi 20. Na pia kuwapa masharti
mapromota wa maeneo ya mbali kumtafutia usafiri wa ndege. Kwa upendo,
wote, wametoa ushauri unaoweza kumjenga japo mwingine unakuwa ni nje ya
uhalisia.
Nakubali kuwa kutokana na alipofika, Darassa hapaswi kulipwa kiasi
kile kile kama ambacho alikuwa anatoza miaka miwili iliyopita, lakini
hilo linapaswa kwenda kwa process. Ni haraka mno kutoka kulipwa mfano
milioni 4 kwa show hadi kuwa milioni 20. Inahitaji justification zaidi
ya kuwa na hits mbili kuweza kulipwa kwa ukubwa huo.
Watu wasimjaze maneno Darassa na kuanza ajisikie kuwa anapaswa kuanza
kuchukua kiasi kile kile ambacho wasanii kama Diamond au Alikiba
wanachukua – kumbuka safari ya wawili hawa na nguvu waliyojikusanyia
hadi sasa. Hapo alipofika Darassa, kuna rappers kibao nyuma waliwahi
kufika, lakini hawakulazimisha kupaa juu ghafla na kutaka walipwe
mamilioni ya shilingi ambayo hayaendani na uhalisia.
Huu ndio muda ambao Darassa anaendelea kujijenga kujitengenezea
ukubwa huo wa kutoza fedha nyingi au kuzikataa zile zinazoitwa ‘show za
vichochoroni.’ Kumbuka kabla ya kuachia Muziki, hakuwa na ‘demand’ hiyo
ya hata kuitwa kwenye utitiri wa show hizo. Show za milioni 3, 4 ndizo
zinaweza kumjengea na kumtengenezea mazingira ya kudai shilingi milioni
15 au 20 kwa show moja baadaye. Hizi ni show zinazompa mtaji wa
kujitengenezea himaya yenye nguvu itakayompa kiburi ya kukataa milioni 5
ili alipwe milioni 15.
Kuna wasanii wanaofanya vizuri ambao kupata show ya milioni 2 au 3 ni
ngekewa, haiwezakani Darassa kuzikataa kisa ametoa hit ndani ya mwezi
mmoja. Isitoshe, show za vichochoroni ndizo zinaonesha ukubwa wa msanii
na dalili kuwa muziki wake umefika mbali. Ehh, ndiyo, haiwezekani
kujiita msanii mkubwa wakati unajulikana mjini tu.
Ushauri wangu kwa Darassa ni kwamba aendelee kuwa mnyenyekevu hivyo
hivyo kama alivyo sasa bila kuanza kuweka attitude kuwa hataki kwenda
baadhi ya sehemu ambazo hazifikiki kwa ndege. Wanasema Roma haikujengwa
kwa siku moja, ama hata mbuyu ulianza kama mchicha.. Ni process,
inahitaji muda kutengeneza ukubwa, hauji ndani ya siku moja.